Yashinde mawazo hasi:Jambo la muhimu ili kutunza afya yako ya akili

Sehemu kubwa zaidi katika kuimarisha afya yako ya akili ni uwezo wako wa kukabiliana na hisia mbalimbali na mambo unayoyapitia yawe mabaya au mazuri na njia moja wapo ambayo imeonekana kuwa imara zaidi ni kujaribu kuandika mawazo yako hasa wakati unapitia kipindi kigumu kitaalamu inaitwa “Journalling”. Mbinu hii itakusaidia kuyatoa mawazo hayo kichwani mwako na kuangalia ukweli wake kwani mara nyingi yanaweza kuwa yanakusumbua tu na wala hata sio kweli. Sababu, ubongo kikawaida unapenda sana stori na bila kujali ni za ukweli au za uongo, ubongo una tabia ya kuziamini. Na wakati mwingine stori hizo ni za uongo kwamba labda “wewe ni mbaya”, au “kwamba kila siku wewe ni mtu wa kukosea”, “wewe huwezi kubadilika”. Zote hizi huweza kuaminiwa na ubongo wako na mwisho wa siku zinaanza kukutesa na kukuondolea amani.

Kwa kuwa yanatokea mara kwa mara mawazo hasi na yanasababishwa na mambo mbalimbali, tumia mbinu hii kupambana nayo.

Labda limekujia wazo hili kwamba “wenzangu wote wananichukia”.

Maswali haya manne yanaweza kukusaidia:

Jiulize:

  1. Je, ni kweli? Pima ukweli wa wazo hilo. Je, ni kweli kwamba wenzako wote wanakuchukia? Bila shaka sio kweli; sio wote wanaweza kukuchukia, huo ndio ukweli.
  2. Unajiskiaje ukiwa na wazo hilo kichwani mwako? Unapokuwa na wazo kama hilo la “wenzangu wote wananichukia”, mara nyingi litakufanya ujiskie vibaya, ujiskie mpweke na kujihisi kwamba una shida na huwezi kupendwa ama kukubaliwa na watu.
  3. Unajiskiaje /unakuwa mtu wa aina gani ukiwa huna wazo hilo kichwani? Bila shaka jibu ni kwamba utajiskia vizuri, mwenye furaha zaidi. Kwani kikawaida, wazo huzalisha hisia, hisia huzalisha tabia, na tabia huleta matokeo fulani ambayo yanaweza kuwa mabaya au mazuri. Na kwa upande wa mawazo mabaya, unapoyaruhusu yabaki kichwani, yatakuletea matokeo mabaya katika eneo lolote la maisha yako. Labda utashindwa kufanya kazi vizuri au labda utaogopa kufanya jambo unalolipenda.

Endelea kusoma; swali la mwisho ni la muhimu sana na ni hili hapa:

  1. Geuza wazo la mwanzo kinyume chake. Mfano, hapo juu wazo lilikuwa kwamba “wenzangu wote hawanipendi”. Sio uligeuze kuwa “wenzangu wote wananipenda” kwani sio kweli, ila geuza kuwa “sio wenzangu wote wananichukia, wapo wanaonipenda”. Kwa kufanya hivyo, utakuwa umesaidia kupunguza athari ya mawazo mabaya akilini mwako.

Kumbuka: Ukiyaacha mawazo mabaya yaendelee kuzurura kichwani mwako, itachochea wasiwasi, hofu na huzuni nyingi na itakuzuia kufanya mambo ya muhimu. Hivyo, kila siku piga vita mawazo mabaya 

Health Talks... Welcome to WhatsApp chat
Howdy! How can we help you today?
Type here...